Saturday 9 July 2016

Umhimu wa Roho mtakatifu katika maisha ya Mwamini.

Yohana 14:16-18


 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni, wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”.


Katika somo hili nataka kuandika juu ya kazi za Roho Mtakatifu na kukuonyesha namna unavyoweza kumtumia Roho Mtakataifu kama Msaidizi kupitia kazi zake. Labda niseme kwa lugha hii, kama unataka kuona msaada wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako, ni lazima kwanza uzijue kazi zake, maana kazi zake ndizo zinazotuonyuesha maeneo ya msaada wake, kazi zake ndizo zinazofafanua kwa namna gani Roho Mtakatifu ni Msaidizi.
Roho Mtakatifu ni nani?


Roho Mtakatifu ni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote, anayepatikana kila mahali. Yeye anayo nafsi na ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu. Kusudi kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.


Roho Mtakatifu amemamua kuishi ndani ya mwili wa mtu kwa sababu, Mungu hana namna ya  kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake. (Yohana 14:23, Yohana 14:18, Ufunuo 3:20, 1Wakorinto 3:16-17, 6:19).


Kinachotusaidia kujua kwamba Roho Mtakatifu ana nafsi, ni tabia zake, maana kwenye kila nafsi kuna hisia, nia, kumbukumbu, akili nk. Baadhi ya sifa na tabia za Roho Mtakatifu ni; anapatikana kila mahali (Omnipresence), Zaburi 139:7, ana maarifa/anajua yote (Omniscient, Intelligence), 1 Wakorinto 2:10-11, ni mwenye nguvu zote/wa umilele (Omnipotent), Mwanzo 1:2, ni Mtakatifu, Luka 11:13, ana hisia (Waefeso 4:30, Mwanzo 6:3) – Wala msimuhuzunishe Roho wa Mungu…, Roho yangu haitashindana na Mwanadamu milele, ana nia (will), 1Wakorinto 12:11 – Hutenda kazi kama apendavyo. ( somo litaendelea,) By pastor Philipo


Saturday 15 November 2014

UMHIMU WA MAOMBI KWA MKRISTO WA LEO.

Maombi na umhimu wake mbele za Mungu:

Mungu ameweka ujumbe huu ndani ya moyo wangu na ninaomba nikushirikishe ili uweze kupokea baraka tele zilizomo ndani ya ujumbe huu. Ili uweze kuelewa ni lazima sasa nieleze nini maana ya maombi.
(1) Maombi ni mazungumzo baina ya mtu na Mungu au Mungu na mtu aombaye kwake. Isaya 1;18. Mungu anaongea hapa na akionyesha pia matokeo yake kwa mwombaji ambaye amekubali kwenda mbele za Mungu katika hali ya kusemezana naye.
 (2) Maombi ni kumwita Mungu juu ya shida au tatizo lolote ulilonalo, ukihitaji msaada wa jambo hilo. Yer 33;3.
 (3) Maombi ni kutafuta ufumbuzi katika Mungu juu ya kile unachotaka kuona Mungu anahuska nacho.2Nya7;14, Mt 7;7. Kuna lugha nyingi sana zilizotumika katika Biblia zinazoonyesha maombi kwa maana hizi.
 Kwa kila mwammini mara tu baada ya kuokoka anapaswa kuanza na kujizoeza kuomba kwani ni mhimu sana katika ukuaji wa maisha ya kiroho na ndiyo maana nikichukua mfano kwa mitume, watu waliotembea na Yesu alipokuwa katika mwili, mara tu  alipowaacha waliendelea kukumbuka kile ambacho Yesu alikifundisha na wakaanza kutii na kufanya, Mdo 2;42. Katika Efe6;10-19. Maombi yametanjwa kuwa ni silaha kwa mwamini, kuomba au kusali (maana ni ile ile) ni sharti kuu na jambo la kujumlisha maisha ya imani na ushuhuda wenye matunda kwa mtoto wa Mungu.

Kweli pasipo kuomba maisha ya hapa duniani ni bure kabisa. kuomba ni njia pekee ya kutuunganisha na chemichemi za uzima wa kweli, yaani na Mungu. Wakati wowote maungamo haya yapo, uzima huu wa Mungu unatujia. Maungamo hayo yakiharibika, matokeo ya lazima ni kwamba, mto huu wa kutuletea maji ya uzima na nguvu unakauka. Na hivyo mtu wa ndani aliyetoka kwa Mungu hurudi nyuma na kunyauka pole pole na kushidwa kukua kiroho kabisa.

Kwa sababu hii, tungeweza kudhani kwamba mtu awezaye kuomba sawa sawa, ni yule tu ambaye amekwisha kuunganishwa na chemichemi ya nguvu hiyo, amekwisha kuwa mtoto wa Mungu. Lakini Biblia inaonyesha kwamba hata mtu ambaye hajazaliwa mara ya pili, lakini anamcha Mungu anaweza kumkaribia Mungu kwa njia ya maombi na kwamba Mungu anaweza kusikiliza maombi yake na kuyajibu pia. Lk 18;13-14, Mdo 10;1-4. kujibiwa kwa maombi si thibitisho la kuwa mtoto wa Mungu, bali ni thibitisho la kuwa mchaji wa Mungu tu. Yeye amtafutaye Mungu kwa njia ya kweli ataanza kwa kuomba na kusoma neno lake. Kwa kufanya hayo uhusiano na Mungu huanzishwa na unahitajika kutunzwa.

Maandiko yana tuhimiza kuchunguza jambo hili la maana sana kwa kujiuliza maswali manne:-
                                       (1) Kwa nini kuomba.
                                       (2) Jinsi gani kuomba.
                                       (3) Wakati gani kuomba.
                                       (4) Kwa kusudi gani kuomba.
-; (1) Kwa nini kuomba,
          (a) Mwili ni dhaifu Mt 26;41; kwa maneno haya Bwana mwenyewe alitoa sababu na jibu la swali letu. Dhiki na taabu hufundisha kuomba Zab 50;15. Katika kuomba tunatambua dhiki na kutokuweza kwetu zaidi. Kwa hiyo mara nyingi Mungu mwenyewe anakubali mtu apate dhiki ili amwonyeshe udhaifu wake na kumkumbusha kwamba msaada wa kweli uko kwake. Ayu.33;30,26

Kama Bwana wetu Yesu mwenyewe,  katika siku za mwili wake, alitoa maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi.................... ingawa ni mwana .............. Ebr. 5;7  si zaidi sana sisi tunahitaji na kutegemea hayo!
          (b) kwa sababu adui ana nguvu na vita ni vikali.
Ni mhimu kuelewa kwamba tunashindana na adui mwenye nguvu kuliko mwanadamu wa kawaida ( asiye na nguvu ya Mungu ndani yake) Kwa hiyo kushinda naye kwa nguvu zetu za kawaida ni bure kabisa.  Zaidi ya hayo kushindana naye na kushinda tunaweza kwa njia ya imani tu. ( Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo, Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo bayana ya mambo yasiyoonekana Warumi 10;17, Ebr11;1). Lakini imani hai ni kuunganika na  Mungu kabisa. Kuunganika kwetu na Mungu kunatunzwa kwa njia ya maombi tu.  1Petro 5;8-9, Flp 4;6-7 Kwa sababu hiyo mtume Paul alijumulisha silaha zote kwa vitavkuu ya kutisha katika silaha kubwa inayotajwa mwishoni ....... katika sala, baada ya kuonyesha nguvu ya adui yetu itishayo kwa mwanadamu. Efe, 6;11-12, 13-17,18!!! 

Ushindi mkubwa kabisa katika historia yote na mashindi makubwa mengine yote, hayakupatikana kwa mapanga na baruti bali yalipatikana kwa kukaa magotini (maombi) Mdo12;1-4 (Mateso ya kanisa) Mst 5, Kanisa liliomba kwa nguvu. Mst 6-17 Majibu na matokeo ya maombi kwa kanisa. 

Yawezekana huduma yako, iko gerezani, ndoa yako iko gerezani, masomo yako, yako gerezani, ajira yako iko gerezani, biashara yako, iko gerezani, NK. Fanya kama kanisa lilivyofanya, shirikisha Mchungaji wako, nk ili kuomba pamoja na ninaamini gereza hilo litafunguka katika jina la Yesu Kristo!! Usiogope Bwana yuko pamoja na wewe.
        (c) Kwa sababu Mungu ana hamu ya kusikia sala na maombi ya watoto wake, ana wahimiza kufanya hivyo mara mara. (Zab50;15, Mt 7;7, 2Nyak 16;9, Yn 4;23b!) Zaidi ya hayo Mungu anaziheshimu sala namna hii hata azitie katika vyombo vya dhahabu na kuzipokea pamoja na mziki. Ufu 5;8. 

Maendeleo na matokeo makubwa mbinguni na duniani, Mungu ameyaweka yategemee maombi na sala za watoto wake. (1Fal 18;36-39, 2Fal 6;17, Dan Sura 9-10, Yak5;16-18, Ufu 8;3-8)   
                              Kumbuka   maendeleo makubwa haya yanategemeana.



Ubarikiwe sana kwa kutembelea Blog hii na endelea ili upate mafundisho Kutoka kwa mch Philip Buluba aliye na mzigo wa kupanda makanisa maeneo yasiyo fikiwa na injili hapa Tanzania. Somo hili linaendelea...

Saturday 13 September 2014

Pongenzi kwa askofu Batenzi.

Ninapenda kuchukua nafasi hii Kumshukru sana Mungu kwa ajili ya uongozi mpya wa kitaifa kanisa la Free Pentecostal Church Tanzania (FPCT) uliopatikana leo jioni baada ya kufanyika uchaguzi halali katika bwalo la UDOM Dodoma. Halmashauri kuu ya kanisa taifa, kwa pamoja tumekuwa UDOM toka 9/92014 tukiendelea na semina yenye baraka nyingi sana. Askofu toka Sudani ya Kusini Ngd Daniel amefundisha neno lililokuwa na lengo la kuwafanya watumishi wa Mungu wayaige maisha ya Yusufu mtoto wa Yakobo kwa jinsi alivyokuwa mwaminifu toka kwa familia ya baba yake, nyumba ya Botifa, gerezani na misri pia. Kutikana na neno la Mungu linaonyesha kuwa pote alipo pita Yusufu alikuwa akimwinua Mungu wake.

Hitimisho la semina hii ni uchaguzi wa uongozi wa kitaifa, Hongera David Batenzi kwa kuchaguliwa tena na Mungu ili uweze kuiongoza FPCT kwa miaka mitano. Mungu ana kusudi na wewe, angalia Mungu amekuchagua kuwa mwenyekiti wa CPCT, tena UKIAMKA, Ubarikiwe sana. Hongera Katibu mkuu Elias Shija kwa kuchaguliwa tena. Na wengineo.  Mungu awabariki sana.





Tuesday 29 July 2014

IMANI MUUMBA.


Yesu alisema, tazama mavuno ni mengi ila watenda kazi ni wachache. Kweli nimeamini baada tu ya kuanzaisha kanisa Kasuguti, sasa kanisa linazidi kuongezeka kiidadi. Mungu akubariki kwa maombi yako!!!

Tuesday 10 June 2014

Kwa Neema ya Bwana Nimepanda kanisa jipya tena.

Wafilipi 4:13
Ninayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Kwa wiki tatu sasa ni Mungu ameniwezesha kupanda kanisa jipya katika kijiji cha Kasuguti, kata ya Kasuguti, Tarafa ya Kikombwo wilayani Bunda mkoa wa Mara. Kabla ya kwenda kupanda kanisa hili, nilisikia sauti ndani ya moyo wangu ikiniambia kwenda kuanzisha kazi mpya. Kwa hiyo niliamua kuitii sauti hiyo.

Kwa hatua ya mwanzo niliamua kwenda kumwona mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kasuguti ili kunipa chumba cha darasa kwa ajili ya kukusanyikia humo maana ndio utamaduni wetu katika hali ya mwanzo ya kuanza kanisa jipya maeneo haya. Ninamshukru Mungu Kwa moyo mzuri niliouona kutoka kwa mwalimu huyo, yeye aliniruhusu akasema hawezi kukataa kuruhusu kazi ya Mungu kuanzishwa katika eneo hilo. Hivyo nilianza kupita nyumba hadi nyumba nikiwashuhudia habari za Yesu Kristo.

Kila niliye kutana naye nilimweleza habari za Yesu na wapi tunapatikana kwa ibada. Ibada yangu ya Jpili ya kwanza niliabudu na watu wazima watatu na mtoto mmoja, siku ya Jtano akaongezeke mmoja, na Jpili ya ya tar 8June nikaabuda na watu wazima Tisa na watoto sita. Kweli nimelihakikisha neno la Bwana Yesu aliposema Mavuno ni mengi ila watenda kazi ni wachache na kwamba tumwombe Baba wa mavuno apeleke wavunaji. Ni kweli!!!!

Ndugu mpendwa katika Bwana, ninaomba maombi yako ili Mungu aiinue kazi yake zaidi. Kumbuka Shetani hutamani zaidi kuua hasa kwa kitu kilicho kichanga bado. Wakati Musa alipozaliwa alitafutwa na Farao ili auawe, Yesu alipozaliwa naye alitafutwa na Herode ili auawe na badala yake watoto wengi wakachinjwa. Nk Tuombee ili kufikia maono hapo chini.

Maono yangu kwa kazi hii, Mwaka huu ninatamani nipate pesa kwa ajili ya kununua kiwanja cha kanisa, ikiwezekana tulete mawe, mchanga na tuujenge.  Hagai1:8

Ubarikiwe na Bwana,

Wednesday 28 May 2014

Umezaliwa ili ukue katika Kristo Yesu.

Mara tu baada ya kumwamini Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, huwa tumezaliwa katika ufalme wa Mungu. Yohana 1:12. Tunakuwa hatujui mambo mengi kiroho yaani ni kama mtoto mchanga kimwili asivyoelewa maisha ya kimwili. Neno la Mungu linatueleza, Lakini Kueni katika neema na katika kumjua Bwana wetu na mwokozi Yesu kristo. 2 Petro 3:18.

Hatua mhimu za kufanya ili tukue kiroho.
(1) Lazima tupende mafundisho ya neno la Mungu. 1Petro 2:2, Ebrania 5:12-14.
(2) Tuwa epuke marafiki wasiomcha Mungu. 2Kor 6:14-18
(3) Tuwe watu wa maombi Wafilipi 4:6-7
(4) Tutii neno la Mungu.

Anza kwa kufanya hayo kwanza na Mungu atabadilisha maisha yako.
Ubarikiwe sana!!! Amen

Friday 23 May 2014

Roho ya msamaha ni msingi wa kwenda mbinguni.

Tunapo kuwa tumemwamini Yesu kuwa Bwana na mwokozi wetu, tunakuwa tumetangaza vita na ufalme wa shetani. Hivyo wengi sana shetani atawafanya watufanyie makosa ya makusudi tu, je tuwachukie? Hapana. Tuwapende na kuwaombea, Mfano Yesu Kristo hakupendwa na wote japo alikuwa akifanya mema kwa watu, aliponya wagonjwa, kufufua wafu, vipofu kuona lakini bado walifanyia mabaya mpaka kmwua msalabani. Jambo la ajabu ambalo Yesu alifanya ni kwamba aliwaombea msamaha wote waliomtendea mabaya. Katika Lk 23:34.  Na umhimu wa kusamehe Yesu ali ufundisha sana kwa wanafunzi wake katika Mt 6:24 na ndiyo maana mitume nao waliwafundisha wengine maana tunaona matokeo ya mafundisho yao kwa Stefano alipopigwa mawe kwa sababu ya kuhubiri kabla haja kata roho naye aliomba msamaha kwa wale waliomfanyia kitendo hicho. Mdo7:59-60.

Kwa nini tusahehe, ni kwa sababu sote tumekosa na ili Mungu asamehe makosa yetu ni lazima tuwasamehe wengine makosa yao. Mt 6:24

Nimalize kwa kusema samehe wengine ili ujiwekee akiba ya kumfanya Mungu akusamehe wewe. Na huo ndio mlango wa wewe kuziona baraka za Bwana. Amen!!!